Pages

Friday, April 20, 2012

Dk. Slaa: Nilizuia umwagaji damu 2010


na Sitta Tumma, Geita
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ameeleza namna alivyowazuia Watanzania kushiriki maandamano mazito ambayo yangeweza kusababisha umwagaji damu kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais mwaka 2010.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa Geita katika mkutano uliofanyika katika uwanja wa magereza mkoani hapa, Dk. Slaa alidai kuwa Watanzania wengi walibaini kile alichokiita kitendo cha kuibiwa kura zake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na hivyo walikuwa wakisubiri kauli yake ya kutaka waandamane.

Huku akishangiliwa na maelefu ya wananchi, Slaa Alisema kuwa Watanzania wengi walimwomba atoe kauli na walikuwa tayari kuingia barabarani hadi Ikulu, lakini alikataa ili kunusuru umwagaji damu.

Aliishambulia idara ya usalama wa taifa kwa madai kuwa ilijua namna kura zake zilivyoibiwa, na kwamba kama asingetumia busara za hali ya juu, hali ya nchi ingekuwa tete.

Slaa aliwashambulia wabunge wa CCM kwa kulamba matapishi kwa yale waliyokuwa wakiyakataa yakiwemo ya nchi kuliwa na mafisadi na mambo ya Katiba mpya.

Alisema kwa sasa wabunge wa chama hicho wameanza kuungana na yale yanayosemwa na viongozi wa CHADEMA, jambo linalodhihirisha kuwa CCM imechoka kuongoza nchi.
Alisema wabunge wa chama tawala ni sawa na mavuvuzela kwa kushindwa kuiwajibisha serikali, badala yake wamebakia kupiga kelele tu.

Lema aunguruma
Kwa upande wake, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amemtahadharisha Rais Jakaya Kikwete kwamba asipobadilika kiutendaji na serikali yake isipozuia uporaji wa rasilimali yakiwemo madini, Watanzania watalazimika kuchukua hatua.

Lema alisema uchumi wa nchi umeyumba na rasilimali zinaporwa hovyo na kumtaka Rais achukue hatua za uwajibikaji.

Diwani mwingine atoka CCM
Katika mkutano huo, Diwani wa Kata ya Lugata, wilayani Sengerema Adirian Tizeba (CCM) alitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.

Akizungumza katika mkutano huo, Tibeza alisema amechoka kukitumikia chama kilichobobea kuwakumbatia mafisadi.
“Rais Kikwete alinirubuni Dodoma lakini nimekuja kubaini CCM imekufa na serikali imebaki kulea mafisadi na kuwatelekeza wananchi,” alisema Tizeba.

Kujiunga kwa Tibeza, kumefanya idadi ya madiwani waliojiondoa CCM kufikia watatu ndani ya wiki moja.

0 maoni:

Post a Comment

Labels