MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora, imemthibitisha Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) kuwa mbunge halali wa Muhambwe na hivyo, kukibwaga Chama cha Mapinduzi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya mahakama hiyo kuitupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jamal Tamami.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo Jaji Aishieri Sumari alisema kuwa mahakama yake imethibitisha pasi na kutia shaka kwamba malalamiko ya kupinga matokeo hayo hayakuwa na uthibitisho wowote.
Wakati hukumu hiyo inatolewa mlalamikaji, Jamal Tamim, hakuwepo mahakamani na badala yake aliwakilishwa na wakili wake Elias Hezrom ambaye alisema kuwa kwa sasa hana la kusema kwa kuhusiana na kukata rufaa au kukubalina na hukumu hiyo.
Ezrom alisema kuwa anatarajia kukaa na mteja wake na kuipitia hukumu hiyo kwa makini na kuona hatua gani wanayoweza kuchukua kulingana na hukumu ya Jaji Sumari.
Kwa upande wake Mbunge Felix Mkosamali alisema kuwa ameridhika na hukumu ya Jaji Sumari ambayo imetimiza misingi ya Katiba ibara ya 107 inayosema kuwa mahakama ndiyo chombo pekee ambacho kinaweza kutoa haki.
Mkosamali ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema kuwa hiyo imeonyesha namna ambavyo vyombo vya haki vikiachwa kuwa huru vinaweza kutenda haki kama ambavyo imefanyika kwenye kesi hiyo na kwamba sasa amepata nafasi zaidi ya kuwatumikia wananchi wa jimbo lake katika kuwaletea maendeleo.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Felix Mkosamali aliyekuwa mgombea wa NCCR – Mageuzi alipata kura 25574 dhidi ya kura 15223 alizopata Jamal Tamim aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi.
Katika kesi hiyo Jamal Tamimu Abdallah alilalamika kuwa Mkosamali wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010, alitoa maneno ya kashfa kwenye mikutano mbalimbali kuwa ni jambazi mkata vichwa vya watu, mchuna ngozi za binadamu na kuwa sio Mtanzania bali raia wa Yemeni hali iliyomkosesha ushindi
|
0 maoni:
Post a Comment