Pages

Friday, April 20, 2012

ZITTO ATAKA SAINI ZA WABUNGE 70 KUMNG'OA,MAWAZIRI WATANO WATAKIWA KUJIUZURU, FILIKUNJOMBE ADAI MKULO MWIZI



 


UKUSANYAJI saini za wabunge kwa ajili ya kuwasilisha azimio la kutokuwa na imani na Waziri Mkuu umechangamkiwa lakini kuna mgawanyiko baina ya wabunge wa CCM kwa kuwa baadhi yao wanapinga azimio hilo.

Hadi jana saa 9 alasiri, wabunge watano wa CCM ndiyo walikuwa wamesaini akiwemo Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, aliyesaini akikanusha kutumwa na mtu kwa kusema hana haja na uwaziri, kama ambavyo baadhi ya wabunge walivyowatuhumu kuwa wanaoshinikiza azimio hilo wanataka uwaziri.

Wanaoponda hoja hiyo wanasema haina mashiko, kwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hahusiki na uteuzi wa mawaziri.

Mbunge aliyezungumza hadharani na waandishi akipinga, ni wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) ambaye amemtetea Pinda kwamba ni mtendaji mzuri na hajavunja maadili yoyote kiasi cha kuruhusu hoja ya kumwondoa kuwa na mashiko.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) ndiye aliyeongoza kazi hiyo jana na hadi saa 9, zilishakusanywa saini 66 za wabunge kutoka vyama vyote isipokuwa United Democratic Party (UDP) ambacho mbunge wake ni John Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti.

Akiongozana na Filikunjombe, Zitto aliwaambia waandishi wa habari kwamba hadi muda huo, idadi ya wabunge wa CCM waliosaini ni watano, CUF 12 na wengine ni waTLP, NCCR-Mageuzi na Chadema.

Zitto ambaye alionekana akizungusha karatasi ya kusaini kabla ya kumkabidhi pia Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), awazungushie wabunge, alisema hoja hiyo inayotarajiwa kuwasilishwa kesho kutwa, ni ya wabunge wote huku akisisitiza kwamba si ya upinzani kama inavyoaminika kwa kuwa ilianzia kwa wabunge wa CCM.

“Hii hoja si ya kambi ya upinzani, si hoja ya Zitto, wabunge wa CCM ndio wengi waliolalamika,” alisema Zitto na kusema taarifa zilizopo ni kwamba CUF makao makuu kimewaelekeza wabunge wake wote wasaini.

Hata hivyo, Zitto alitetea udandiaji wa hoja za chama kingine, iwapo zina maslahi kwa wananchi na Taifa. “Katika siasa za kibunge, anayesema hoja imedandiwa, amefilisika…mimi sijafanya hili kama Mbunge wa Chadema. Kuna ubaya gani kama CCM au Chadema ina hoja nzuri mtu kuidandia?” Alihoji.

Zitto ambaye ndiye aliwasilisha juzi bungeni wazo la kuunda azimio hilo, alisisitiza kwamba wabunge wanampenda Pinda isipokuwa mawaziri wake ndio wamemweka rehani iwapo hadi keshokutwa watakuwa hawajachukua hatua za kujiuzulu.

“Tunampenda na kumheshimu sana Waziri Mkuu, lakini pia tunaiheshimu nchi yetu,” alisema na kuongeza kwamba kumpigia kura hiyo, kutaweka historia ndani ya nchi kwani tangu uhuru, hatua kama hiyo haijapata kuchukuliwa. Alipoulizwa kuwa iwapo hoja yao haitapitishwa ni hatua gani watachukua, Zitto alisema Bunge litaingia kwenye historia kwa kuonesha meno.

Taarifa ambazo zimekuwa zikisambazwa, ni kwamba lipo kundi linawatumia baadhi ya wabunge kushinikiza hoja hiyo ipite. “Kuna Mbunge anasambaza uvumi, kwamba watu wamewatuma walete hayo…tusipowawajibishe, wananchi watatudhihaki, tunalinda heshima ya Bunge,” alisema Zitto.

Kwa upande wake, Filikunjombe ambaye alisema baadhi ya wabunge akiwamo yeye, waliitwa jana kushawishiwa kuondokana na kusudio hilo, lakini akawaambia waandishi wa habari kwamba hana mpango wowote wa kutaka kuwa waziri na ikitokea jina lake limewekwa kwenye orodha, ataomba liondolewe.

Msimamo wa wabunge waliosaini ni kwamba lengo la azimio hilo ni kutoka kwenye Bunge la ulalamikaji kwenda Bunge la utendaji ama kwa Waziri Mkuu kuwapisha au kuwawajibisha mawaziri wasiofaa kutokana na ama kuhusika katika ubadhirifu au kushindwa kuudhibiti.

Hoja ya azimio hilo iliwasilishwa juzi baada ya wabunge wengi kuchangia ripoti za kamati za Bunge, wakiwashutumu baadhi ya mawaziri kuwa watafunaji wa mali za Serikali kwa kutaka wawajibishwe.

Sendeka alisema katika mapendekezo yaliyoafikiwa juzi hakuna azimio katika kamati yoyote la kutaka waziri aondolewe na kusema kuwa alichokuwa akikifanya Zitto ni usanii.

Kwa mujibu wa Sendeka, katika taarifa ya Zitto alipaswa aseme Bunge limependekeza mtu fulani awajibishwe.

“Hivyo alitakiwa kuleta nyongeza katika taarifa yake. Hakuna aliyeleta. Ile ni burudani tu,” alisema na kuongeza kuwa hoja hiyo haina mashiko.

Alihoji kuwa iwapo Pinda alishindwa kumwondoa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, atawezaje kumwondoa Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo.

Alisema ili hoja hiyo ifanikiwe, ni lazima Spika aridhike, kwamba ilifuata taratibu na kuongeza kuwa hata ikisainiwa na wabunge 200 kama haina sifa haiwezi kupita. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, kifungu cha 133 kinazungumzia hatua zinazopaswa kufuatwa ili kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Inasema ili hoja ya kutaka kupitisha Azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu inapaswa isiwe na uhusiano na utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu yaliyoainishwa katika Ibara 52 ya Katiba.

Hoja haitatolewa iwapo hakuna madai kwamba Waziri Mkuu amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Pia haiwezi kuruhusiwa iwapo haijapita miezi tisa tangu hoja ya namna hiyo ilipotolewa bungeni na Bunge likakataa kuipitisha.

Kifungu hicho kinaelekeza pia, kwamba hoja hiyo haitajadiliwa na Bunge isipokuwa tu kama taarifa ya maandishi iliyosainiwa na kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 itatolewa kwa Spika, siku zisizopungua 14 kabla ya siku inayokusudiwa kuwasilishwa bungeni.

Chini ya kifungu hicho, hoja itapitishwa iwapo itaungwa mkono na wabunge wengi. Endapo itapitishwa kwa kupigiwa kura za siri, Spika atawasilisha azimio husika kwa Rais. Waziri Mkuu atajiuzulu na Rais atateua Mbunge mwingine kuwa Waziri Mkuu.



habari kwa hisani ya Gazeti la HabariLeo

0 maoni:

Post a Comment

Labels