Pages

Tuesday, May 14, 2013

FAINALI YA THE MIC KING KUFANYIKA MEI 25

FAINALI ya shindano la Hip Hop la The Mic King ambalo linaratibiwa na Ukumbi wa Dar Live, Litafanyika Mei 25, mwaka huu, na mshindi atazawadiwa gari aina ya Toyota Fun Cargo.

Kwa mujibu wa Luqman Maloto ambaye ni mratibu wa shindano hilo, fainali ya The Mic King itafanyika siku hiyo katika kilele cha Usiku wa Hip Hop ambao huandaliwa na Ukumbi wa Dar Live, ulioko Mbagala Zakhem, Dar es Salaam.


“Usiku wa Hip Hop hufanyika kila mwaka kwenye ukumbi wetu wa Dar Live ambao ni uwanja wa taifa wa burudani, sasa kwa vile shindano lenyewe ni la muziki wa hip hop, sasa tukaona lazima fainali iwe ndani ya kilele cha Usiku wa Hip Hop.

“Kwa watu waliohudhuria Dar Live mwaka jana Machi 4, watakuwa mashahidi kwamba Usiku wa Hip Hop ni mkubwa sana. Ndiyo usiku wenye kumbukumbu ya kweli ya Hip Hop, wanaharakati wa muziki huo hukumbukwa.

“Kuna wanamuziki wengi wa hip hop wameshatangulia mbele ya haki, siku hiyo watakumbukwa. Tutawasha mishumaa, kuwapigia saluti na kuwaombea mapumziko mema huko waliko,” alisema Luqman na kuongeza: “Kutakuwa na tuzo za hip hop kwa wanamuziki waliofanya vizuri mwaka uliopita. Tutatoa tuzo kwa Wimbo Bora wa Hip Hop, Mwanamuziki Bora wa Hip Hop na Chipukizi Bora wa Hip Hop.”

Luqman aliongeza kuwa baada ya washiriki tisa kuchuana na kumpata mshindi atakayezawadiwa gari, wakali wa Hip Hop Tanzania, Fid Q, Joh Makini, Ney Wamitego, Stamina na Kala Jeremiah watashusha burudani yenye ujazo mkubwa.

0 maoni:

Post a Comment

Labels