MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na
kampuni za simu na vyombo vya usalama imeanza kampeni endelevu yenye
lengo la kuwabaini wote wanaotumia namba za simu bila kusajiliwa.
Kampeni hiyo itasaidia kulinda watumiaji wema wa simu na jamii kwa
ujumla kwa ajili ya kuimarisha usalama na kuleta maendeleo na ustawi wa
wananchi.
Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari iliyotolewa jijini Dar es
Salaam juzi ilieleza ni kosa la jinai kwa watumiaji, watoa huduma na
wakala wa kampuni za simu kutumia namba za simu ambazo hazijasajiliwa.
Taarifa hiyo iliwataka wote ambao hawajasajili namba zao za simu
kufanya usajili mapema ukihusisha taarifa sahihi za mtumiaji, kwani
adhabu kwa wasiosajili ni kutozwa faini ya sh 500,000 au kufungwa miezi
mitatu jela.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza katika vikao vya pamoja vilivyofanyika
kati ya Aprili 4 hadi 11 kwa kushirikisha TCRA, Airtel, BOL, MIC (TIGO),
Sasatel, TTCL na Vodacom wamekubaliana kwa pamoja kumaliza tatizo la
usajili wa namba za simu na kuazimia kufungia namba zote za simu
ambazo hazikusajiliwa.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 130 cha sheria ya Mawasiliano ya
Elektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, mtu yeyote ambaye anauza au
anatoa kwa namna yoyote ile namba ya simu bila kuisajili anatenda kosa
la jinai na adhabu yake ni faini ya shilingi 3,000,000 au kifungo cha
miezi 12 au vyote,” ilieleza taarifa hiyo.
0 maoni:
Post a Comment