Na Elizabeth John
MUIGIZAJI wa filamu za kibongo na mchekeshaji, Tumaini Martin
‘Matumaini’ ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam
ambako anatarajiwa kurejea tena baada ya kumaliza dozi ya dawa
alizopewa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, rafiki wa karibu wa msanii huyo,
Robert Kiwewe ‘Kiwewe’ alisema kuwa, Matumaini alilazwa hospitalini hapo
kwa siku tatu akiwa anasumbuliwa na miguu, ambako juzi aliruhusiwa
kurudi nyumbani.
“Hivi nimetoka nyumbani kwao Yombo kumuangalia, bado hali yake sio
nzuri, daktari kampa dawa, kamwambia arudi hospitali baada ya kumaliza
kumeza dawa hizo, Watanzania tunatakiwa kumuombea mwenzetu ili arudi
katika hali yake ya kawaida,” alisema Kiwewe.
Alisema hali yake sio nzuri, kwani hadi sasa hajui ugonjwa unaomsumbua,
taarifa walizozipata mwanzo ni kwamba alianza kusumbuliwa miguu,
ikafuata na mikono na sasa maumivu yamesambaa sehemu mbalimbali za mwili
wake.
Kiwewe alisema kuwa, kutokana na kushindwa kugundua ugonjwa unaomsumbua, daktari ameamua kumpa dawa za kupunguza maumivu.
Alisema kwa sasa hawana utaratibu mwingine ambao wameweza kuufanya hadi amalize kumeza dawa hizo na kurejea tena hospitali.
Matumaini alikwenda kuishi nchini Msumbiji na kuripotiwa kusumbuliwa na
maradhi, lakini alishindwa kutibiwa akiwa huko ambako Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla akishirikiana na
baadhi ya wasanii, alichukua jukumu la kutoa nauli ya kumrudisha nchini.
0 maoni:
Post a Comment