Mwanafunzi
wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Tegeta jijini Dar es
Salaam, Bertha Amir (14), pichani, amejinyonga hadi kufa akipinga
kulazimishwa na mama yake mzazi kusoma.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema mwanafunzi huyo
alijinyonga juzi saa 11:00 jioni, maeneo ya Tegeta Namanga, jijini Dar
es Salaam.
Alisema marehemu alikutwa amejinyonga chumbani kwa kutumia mtandio ulioning’inizwa juu ya dari.
Kamanda
Wambura alisema sababu za mwanafunzi huyo kujinyonga bado
hazijafahamika, lakini akasema inasadikika kuwa wakati wa enzi za uhai
wake, siku moja kabla ya kifo chake, alikuwa ameongea na mama yake,
Angelina Maiko Mshami (30), ambaye alimtaka achukue fedha kwa ajili ya
kujiandaa kwenda shule.
Alisema mtoto huyo alimjibu mama yake kuwa hahitaji kusoma, bali anataka kufanya kazi.
Kamanda
alisema kuwa mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya
Mwananyamala kwa uchunguzi na kwamba, polisi wanaendelea na upelelezi
kuhusiana na kifo chake.
Mama
wa mtoto huyo, Angelina Mshami, alisema alishangazwa na kitendo cha
mtoto wake kuamua kukataa shule ghafla wakati alikuwa ana uwezo mzuri
darasani.
Alisema
kuwa mtoto wake alikuwa na akili darasani akishika nafasi ya kwanza ama
ya pili wakati akisoma shule ya msingi na hivyo kumfanya afaulu
kujiunga kidato cha kwanza.
Hata hivyo, alisema kabla ya kifo chake, binti yake alimweleza kuwa hataki shule bali anataka kufanya kazi.
Alisema alipomuuliza kazi gani anataka kuifanya, hakuitaja bali alisisitiza kuwa anaifahamu mwenyewe.
Betha ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wawili katika familia yao, alizaliwa mwaka 1999, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
Alianza
darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Malindi mkoani Tanga na
kufanikiwa kujiunga na Shule ya Sekondari Mtumbi na baadaye kuhamishiwa
katika Shule ya Sekondari Tegeta.
Aidha, baadhi ya majirani waliokuwapo msibani hapo, walielezea masikitiko yao na huzuni kuhusiana na kifo cha msichana huyo.
Marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo kuelekea mkoani Tanga kwa mazishi yatakayofanyika kesho kijijini Malindi
0 maoni:
Post a Comment