Madaktari
wanaomtibu Nelson Mandela wameishauri familia yake iondoe mashine
zinazomsaidia kupumua kwani ‘asingeweza kuendelea kuishi’.
Taarifa hizo zimo kwenye viapo vya
wanafamilia hao ambavyo viliwasilishwa katika Mahakama Kuu ya Eastern
Cape, Mthatha ambako familia hiyo ilikuwa ikipambana kurejesha mabaki ya
miili ya watoto wa Mandela kutoka Mvezo kwenda Qunu.
Wanafamilia 16 walifungua kesi
mahakamani akiwemo mkewe Graca Simbine Machel Mandela na mtalaka wake
Winnie Madikele Mandela dhidi ya walalamikiwa watatu akiwemo Zwelivelile
Mandle Sizwe Dalibhenga, maarufu Mandla, ambaye ni mjukuu wa Mandela.
Mandela ambaye aliongoza vita ya
ubaguzi wa rangi enzi za utawala wa mabavu wa Makaburu, alilazwa tangu
Juni 8 mwaka huu katika hospitali ya magonjwa ya moyo, Medclinic iliyopo
Pretoria ambako hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya sana.
Juzi na jana afya ya kiongozi huyo
ilizua utata na mvutano mkubwa kutokana na kutolewa kwa taarifa kwamba
madaktari wanaomtibu walishauri familia yake iondoe mashine
zinazomsaidia kupumua kwani ‘asingeweza kuendelea kuishi’.
Hati za viapo hivyo zinathibitisha
kwamba Mandela anapumua kwa mashine na madaktari wanaomtibu waliishauri
familia kuondoa mashine hizo suala ambalo limebaki katika mikono ya
familia.
Viapo hivyo viliandikwa Juni 26 mwaka
huu na kuwasilishwa mahakamani Juni 28, lakini havikuwahi kutolewa
hadharani hadi Julai 3, wakati uamuzi wa kesi ulipotolewa na kumwamuru
mjukuu wa Mandela, Mandla arejeshe mabaki ya miili ya watoto wa babu
yake Qunu.
Mabaki hayo yaliyohamishiwa Mvezo
2011 ni ya watoto wa Mandela ambao ni Madiba Thembekile aliyefariki kwa
ajali ya gari 1969, Makgatho aliyefariki 2005 na binti yake wa kwanza
Makaziwe (mkubwa) aliyefariki dunia 1948 akiwa mtoto mchanga.
Mabaki hayo yalizikwa juzi Alhamisi katika makaburi ya familia, Qunu ikiwa ni utekelezaji wa amri ya mahakama.
Kati ya juzi na jana, Ikulu ya
Pretoria ililazimika kutoa taarifa mbili; moja muda wa jioni na nyingine
usiku wa kuamkia jana ikiwa ni hatua ya kuondoa hofu iliyokuwa imeanza
kusambaa baada ya vyombo vya habari kuweka bayana kilichoandikwa katika
viapo vya mahakama.
Hoja kubwa ambayo imekuwa ikijadiliwa
ni kwa jinsi gani viapo vya mahakama vionyeshe kwamba uwezekano wa
Mandela kuendelea kuishi ni mdogo huku Serikali ikitoa taarifa kwamba
hali ya Mandela ni imara licha ya kwamba yu mahututi.
Katika taarifa zote mbili Rais Jacob
Zuma kupitia kwa msemaji wake, Mac Maharaj aliweka wazi kwamba Mandela
‘siyo mtu wa kufa wakati wowote’ kama ilivyoripotiwa ikasisitiza kwamba
hali yake imeendelea kuwa imara licha ya kwamba ni mgonjwa sana.
MWANANCHI
0 maoni:
Post a Comment