JIJI la Dar es Salaam leo litakuwa kwenye heka heka kubwa za
kumpokea Rais wa Marekani, Barrack Obama anayetarajia kuwasili saa nane
mchana.
Ujio wa kiongozi huyo umesababisha kufungwa kwa barabara na kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo mbalimbali.
Kwa takribani wiki moja sasa ulinzi umeendelea kuimarishwa zaidi kwa
kuwashirikisha makachero wa Marekani wakiwemo FBI, CIA na wale wa
Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Obama anayeongozana na familia yake
anatarajiwa kupokelewa jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais
Jakaya Kikwete na baadaye atakwenda Ikulu kwa mazungumzo rasmi.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa Obama atapata fursa ya kufanya mkutano
na wafanyabiashara Ikulu pamoja na kuhudhuria dhifa ya kitaifa.
Kesho atakwenda kutembelea mitambo ya kufua umeme ya Symbion iliyopo
Ubungo, Dar es Salaam na kuzindua rasmi Mpango Maalum wa Maendeleo ya
Nishati Barani Afrika ulioanzishwa na Marekani wa Power Africa Initiative.
Kutokana na ujio huo wa Obama, maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es
Salaam yalikuwa na ulinzi mkali wa makachero wa Marekani na Tanzania
pamoja na barabara atakazopita kiongozi huyo kufanyiwa usafi.
Barabara atakazopita Obama pia zimefanyiwa matengenezo madogo madogo
hususani zile zilizokuwa na mashimo, huku nyingine zikiwekewa taa za
barabarani pamoja na bendera za mataifa hayo mawili.
Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao pembeni
mwa barabara anazopita kiongozi huyo, wamehamishwa na usafi umekuwa
ukifanyika kwa kiwango cha juu.
Katika viwanja vya Karimjee ambako kulikuwa kukitolewa vitambulisho
vya watu watakaoshiriki kwenye matukio hayo, kulikuwa na idadi kubwa ya
magari ya kisasa yatakayowabeba.
Magari hayo mengi yakiwa ni mabasi madogo, yalikuwa na bendera za
Marekani na maandishi maalumu ya kuelekeza ni watu wa aina gani
wanaopaswa kuyatumia.
Mpango wa nishati ya umeme
Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi saba ambazo zinatarajiwa
kufaidika na ziara ya Rais Obama katika mpango wake maalumu wa
maendeleo ya nishati barani Afrika ulioanzishwa na nchi yake wa ‘Power
Africa Initiative’.
Mpango huo utazinduliwa kesho na Rais Obama anayetarajiwa kuwasili nchini leo kwa ziara ya siku mbili.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, jana jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa nchi nyingine
zinazotarajiwa kufaidika na mpango huo utakaogharimu dola bilioni 7
katika awamu ya kwanza mbali na Tanzania, ni Ethiopia, Kenya, Liberia,
Nigeria, Uganda na Msumbiji.
Taarifa hiyo ilielezea sababu za nchi hizo kuchaguliwa ni kutokana na
malengo yao kabambe ya kufanya mageuzi ya sekta ya nishati kwa ajili
ya kusafisha njia kwa ajili ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Taarifa ya Ikulu ya Marekani
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, ilielezea kuanzishwa kwa
Mpango wa Maendeleo ya Nishati barani Afrika kumechangiwa na wakazi
wengi kukosa huduma hiyo.
Taarifa hiyo imesema kuwa “zaidi ya mbili ya tatu ya watu wanaoishi
kusini mwa jangwa la Sahara hawana huduma za umeme, na wengine zaidi ya
asilimia 85 wanaoishi maeneo ya vijijini hawapati huduma ya umeme.”
Ilisema kuwa mpango huo kwa eneo la nchi za kusini mwa Jangwa la
Sahara unahitaji zaidi ya dola bilioni 300 kwa ajili ya kukamilika hadi
ifikapo mwaka 2030.
Obama yuko katika ziara ya Afrika akiwa tayari ametembelea nchi za
Senegal na Afrika Kusini na leo anatarajiwa kumalizia nchini Tanzania.
Akiwa Senegal
Akiwa katika ziara yake nchini Senegal, Obama alijikuta katika
wakati mgumu kutokana na mwenyeji wake, Rais Macky Sall kupinga kauli
yake ya kumtaka kurekebisha sheria zao za kutoa haki kwa makundi ya
mashoga.
Rais huyo alipinga kauli hiyo, mbele ya wanahabari ambako alisema;
“ingawa Senegal ni nchi tulivu sana, lakini haiko tayari kuruhusu
maingiliano ya ngono kati ya watu wenye jinsia moja, na hatuko tayari
kubadili sheria kwa ajili ya kuwatambua kwa sababu nchi hii watu wake
wengi ni waumini wa dini ya Kiislamu ambao wanakataa kusikia hilo
likitokea.”
Baada ya kuona sheria yake imeshindwa kupenya, Obama alisema kuwa nia
yake katika mkutano huo haikuwa kufanya majadiliano ya suala hilo na
Sall.
Afrika Kusini
Akiwa Afrika Kusini, Obama alipata fursa ya kuzungumza na rais wa
nchi hiyo, Jacob Zuma. Pia alimtakia afya njema mpigania haki za watu
weusi, Nelson Mandela ambaye kwa sasa amelazwa katika hospitali ya
Pretoria nchini Afrika Kusini kwa muda wa wiki tatu sasa.
Alitoa wito kwa viongozi wa Afrika na duniani kwa jumla kufuata mfano
wa rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini, kwa kulitanguliza mbele taifa
zaidi ya nafsi yake.
Obama alisema viongozi wanaoshikilia nyadhifa hizo kwa muda
wanatakiwa kutodanganyika na kujua kuwa hatima ya nchi zao haitegemei
watakavyoendelea kuwa madarakani.
Akiwa nchini humo, alipata nafasi ya kuwajulia hali ndugu wa Mandela
ikiwa ni pamoja na jana kutembelea katika kisiwa cha Robben, ambako
Mandela alifungwa kwa muda wa miaka 18 kati 27 aliyokuwa amehukumiwa.
Baada ya hapo alizungumza na wananchi wa Afrika Kusini kupitia Chuo Kikuu cha Cape Town.
Akiwa nchini humo alieleza kuwa amekuja Afrika kwa dhumuni la
kusaidia uwekezaji, sekta ya afya ikiwamo na kukuza demokrasia.
Akizungumzia kuhusu China, alisema kuwa hana tabu nao katika
uwekezaji wao kwa nchi za Afrika ambako imefanikiwa kuwekeza kwa zaidi
ya mabilioni ya dola ikilinganishwa na wao Marekani ambao hawajawekeza
kwa kiasi kama hicho.
Obama ameisifia China kwa kuwekeza Afrika, lakini alitoa angalizo
kwamba wasitumie fursa hiyo kwa kujinufaisha wenyewe na badala yake
wawanufaishe na Waafrika kiuchumi kutokana na uwekezaji huo.
0 maoni:
Post a Comment