Handeni Tanga.
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, Bibi Harusi ambaye ni mkazi wa Chanika mjini
Handeni, Levina Mmasi (23) amefariki dunia saa moja kabla ya ndoa yake
kufungwa katika Kanisa la Katoliki la Roma Wilaya Handeni Jumamosi na
hivyo kuilazimu kamati ya maandalizi ya harusi kujigeuza na kuwa ya
msiba.
Kifo hicho kilichotokea Jumamosi mwishoni
mwa wiki iliyopita, kimekuwa gumzo mjini Handeni huku wananchi wakisema
kuwa ni tukio ambalo halijawahi kutokea katika wilaya hiyo.
Marehemu Levina Mmasi akilishwa chakula na aliyetarajia kumuoa,
Kasisi Masawe kwenye hafla ya kuagwa kwake (Send-Off Party) iliyofanyika
Jumatano iliyopita.
Msemaji
wa familia ya marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Firmin Mrimasha,
alisema kuwa chanzo cha kifo cha Levina ambaye alijifungua mwanzoni mwa
wiki iliyopita,ilikuwa ni homa aliyoipata ghafla siku ya Alhamisi na
kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni na kukutwa na malaria na
kisha kulazwa kwa matibu.
“Huyu
bibi harusi alikuwa ametoka kujifungua, alikuwa na mtoto wa kiume
kutokana na ujauzito wa miezi saba, ndipo ghafla Alhamisi akapata homa
tukampeleka hospitali alikolazwa na baada ya kupata nafuu, aliruhusiwa
Ijumaa.
“Baada ya kuruhusiwa akaanza maandalizi ya
harusi na Jumamosi ambayo ndiyo siku ya ndoa yake, alijiandaa lakini
ilipofika saa 8.05 akafariki dunia akiwa nyumbani akisubiriwa kwenda
kanisani kufunga ndoa ambayo ilikuwa ifungwe saa 9.00,” alisema
Mrimasha.
Alisema, “Inasikitisha sana ila
imeshatokea yaani marehemu amefariki saa moja kabla ya ndoa yake na
baada ya kifo hicho, mtoto wake naye alifariki muda mfupi baada ya mama
yake kufariki dunia,” alisema Mrimasha.
Akizungumzia
mkasa huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Harusi hiyo iliyogharimu Sh7.7
milioni, Abdi Kipacha alisema kuwa kwake ni tukio la kwanza kutokea
tangu kuzaliwa kwake na kamwe hawezi kulisahau.
“Nilishazipangia
kazi kamati za maandalizi, lakini ghafla tukapewa taarifa kuwa bibi
harusi amefariki...Hatukuamini, ikabidi niwatangazie wanakamati wenzangu
kuwa hakuna tena shughuli, bibi harusi amefariki,” alisema mwenyekiti
huyo wa kamati na kuongeza:
“Kitu tulichokuwa
tukisubiri ni kuambiwa bibi harusi angefika saa ngapi, lakini ghafla
tukapewa taarifa za kifo, ilikuwa ni vigumu kuamini lakini ni kweli
imetokea na inasikitisha kwani si jambo la kawaida,” alisema Kipacha.
Kwa
mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wanandugu ni kuwa marehemu alikuwa
Mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi na kwamba alikuwa katika
kundi la walimu wa ajira mpya ambayo hadi mauti yanamkuta alikuwa
hajapokea hata mshahara wake wa awali.
Akizungumzia
hali hiyo, Padri aliyekuwa afungishe ndoa hiyo, Max Sabuni wa kanisa
hilo Katoliki Handeni alisema: “Nimesikitishwa na tukio hili kwa
kuwa halikuwahi kunitokea...Kilichobaki ni wanandugu kuwa watulivu kwa
kuwa Mungu amechukua kiumbe wake kwa muda alioupanga.”
Aliwataka ndugu, jamaa na marafiki kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi.
Naye
mume wa marehemu, Kasisi Masawe alisema: “Nimechanganyikiwa sana na
hili...Ni jambo ambalo sikulitarajia. Ninamshukuru Mungu kwa yote
japokuwa kifo hiki kimeniharibia mipango yangu mingi ya maisha na
Levina.
“Nilipanga mengi na yeye, lakini Mungu
hakupenda...Nilimpenda sana Levina,leo ameniacha. Amekwenda na
mwanangu...Ni pigo kubwa kwa kweli, mke na mtoto kwa wakati mmoja,
inauma sana.”
Mwili wa bibi harusi huyo
ulisafirishwa jana kupelekwa Machame mkoani Kilimanjaro kwa maziko
ambayo yanafanyika leo Jumatano pamoja na mtoto wake ambaye naye
alifariki saa chache baada ya mama yake.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alithibitisha kutokea tukio
hilo lakini akasema hawezi kuzungumzia kwa undani kwa kuwa ni tukio la
kifamilia zaidi.
0 maoni:
Post a Comment