MSANII wa kimataifa wa Tanzania, Naseeb Abdul, ‘Diamond Platnumz’ anatarajia kufanya usaili kwa ajili ya watu watakaotumika kurekodi video ya wimbo wake mpya ambao utaachiwa hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Kampuni ya One Touch Solutions, Petter Mwendapole, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa Diamond amefikia uamuzi huo katika kuhakikisha kazi zake zinafanyika katika kiwango cha kimataifa.
“Jumamosi ijayo tutafanya usaili wa watu ambao wataonekana kwenye video hiyo, hii ni mara ya kwanza kwa kitu kama hiki kufanyika nchini kwetu, ingawa wenzetu Ulaya wamekuwa wanafanya hivyo na wanaonekana wanakuwa wanalipwa tofauti na video nyingi za wasanii wa hapa kwetu, na hao watakaochaguliwa kwenye video hiyo watalipwa pia,” alisema.
Akizungumzia kuhusu video hiyo, Mwendapole alisema, itarekodiwa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya soko ambalo msanii huyo analiangalia kwa sasa, huku video hiyo ikitengenezwa na kampuni bora kabisa Tanzania.
Kwa upande wake, Diamond alisema, lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuleta mapinduzi katika sekta ya muziki nchini, lakini pia kutengeneza ajira kwa ajili ya wasichana na wavulana ambao wako mitaani lakini wanapenda muziki.
Diamond ambaye alikuwa nchini Marekani wiki iliyopita, anatarajiwa kwenda tena huko kwa ajili ya onesho moja la muziki.
Msanii huyo alifanya mapinduzi katika medani ya muziki wa bongo, baada ya kufanya onesho lake alilolipa jina la ‘Diamond’s are Forever’ Mlimani City, ambako shoo hiyo aliifanya mwenyewe na kiingilio kikiwa sh 50,000, jambo ambalo halijawahi kufanyika katika ulimwengu wa muziki nchini.
0 maoni:
Post a Comment