MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu, aliyekuwa
anakabiliwa na mashitaka ya kumuua msanii mwenzake Steven Kanumba kwa
kukusudia, amebadilishiwa hati ya mashitaka na sasa anashitakiwa kwa
kosa la kuua bila kukusudia.
Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo
iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.
Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga alidai kuwa upelelezi umekamilika
ambapo mahakama imepanga Desemba 21, mwaka huu kumsomea Lulu maelezo ya
kesi pamoja na ushahidi ambao upande wa mashitaka utautumia katika kesi
hiyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika
hatua ya upelelezi na sasa itahamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza
kusikilizwa ambapo mshitakiwa ataruhusiwa kujibu mashitaka dhidi yake.
Kwa mujibu wa sheria, kutokana na Lulu kushitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, anaweza kupata dhamana.
Lulu aliposikia kuwa upelelezi wa kesi yake umekamilika alifurahi na
kuanza kucheza kwenye kiti na alipotoka katika chumba cha mahakama,
aliendelea kucheza huku akirukaruka.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu nyumbani Steven
Kanumba, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua msanii huyo
nyota wa filamu nchini.
Hata hivyo, kabla kesi haijaanza kusikilizwa, tayari ilishafika
Mahakama ya Rufani, baada ya kuibuka kwa utata wa umri wa mshitakiwa
huyo.
Utata huo uliibuka baada ya mawakili wanaomtetea msanii huyo, kuomba
kesi hiyo isikilizwe katika Mahakama ya Watoto kwa madai kuwa Lulu bado
mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama inavyoonesha katika
hati ya mashitaka.
Mahakama Kuu ilikubali kuchunguzwa kwa umri wa Lulu, lakini Mahakama
ya Rufani ilitengua uamuzi huo na kuamuru kesi ya msingi iliyofunguliwa
Mahakama ya Kisutu kuendelea.
0 maoni:
Post a Comment