Pages

Tuesday, August 20, 2013

BILIONEA WA HOME SHOPPING CENTRE ASHINDIKANA KUTIBIWA

Hakika aliyemmwagia tindikali bilionea Said Mohamed Saad, alifanya kitendo kibaya kupitiliza, kwani athari ambazo amemsababishia ni kubwa kiasi ambacho hata upatikanaji wa tiba mahsusi umekuwa wa kutangatanga. 

Gazeti hili linazo taarifa za ndani na zenye uhakika kuwa Said ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Home Shopping Centre, amekimbizwa Ujerumani kwa matibabu zaidi baada ya kushindikana Afrika Kusini alikopelekwa awali.

Said alimwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu, mishale ya saa 2 usiku akiwa kwenye moja ya maduka yake yaliyopo kwenye jengo analodaiwa kulimiliki la Msasani Mall.

Ilielezwa kuwa baada ya kumwagiwa tindikali, alikimbizwa kwenye Hospitali ya Ami Wellness Centre iliyopo Masaki, Dar es Salaam lakini ndani ya kipindi kisichozidi dakika 60, alichukuliwa na kupandishwa ndege kupelekwa Afrika Kusini.

AFRIKA KUSINI MATUMAINI KIDOGO

Ndugu wa Said aliyeomba hifadhi ya jina lake gazetini, alisema kuwa akiwa Afrika Kusini, ilionekana kwamba bilionea huyo anatakiwa kufanyiwa oparesheni ya uso ili kuondoa ngozi iliyoathiriwa na tindikali, vilevile kulifanyia jicho upasuaji.

“Sehemu ya usoni kushuka kifuani upande wa kulia na mkono wenyewe wa kulia ndiyo maeneo katika mwili wa ndugu yetu yaliyoathirika zaidi na tindikali,” alisema ndugu huyo wa ndani kabisa kwa sharti la kutotajwa jina na kuongeza:

“Jicho la kulia lenyewe limepata athari kidogo, kwani inaonekana wakati mmwagaji akifanya kile kitendo, yeye alifumba macho kwa hiyo tindikali haikuingia ndani ya jicho, iliishia kwa juu.

“Ila kwa vile tindikali ilimwagika kwa wingi juu kwenye jicho la kulia na kutokana na ukali wa tindikali aliyomwagiwa, imesababisha kutengenezwa kwa mtoto wa jicho kwa hiyo hawezi kuona mbali.

“Uamuzi wa kumpeleka Ujerumani uliafikiwa baada ya kujiridhisha kwamba kule kuna wataalamu kuliko Afrika Kusini. 
 
Oparesheni ya uso kubadili ngozi iliyoathirika, vilevile kufanya upasuaji wa jicho na kuliweka sawa ni mambo ambayo tulijiridhisha yanawezekana Ujerumani.”

AKATAA KUTAJA JINA LA HOSPITALI

Kwa mujibu wa ndugu huyo, Said aliondolewa Afrika Kusini na kupelekwa Ujerumani, Agosti 3, mwaka huu na tangu hapo taarifa zake zimefanywa siri kubwa ili kulinda usalama wake.

“Hata wakati nazungumza na wewe kama mwandishi wa habari, nilijua tu lazima utaniuliza kuhusu jina la hospitali aliyolazwa Ujerumani. Ukweli ni kwamba siwezi kukwambia. 
 
Tunafanya hivyo kwa ajili ya usalama wa ndugu yetu.

“Tukio la kumwagiwa tindikali ni zito sana, imeshajionesha wazi namna ambavyo kuna watu hawampendi, hao maadui wakijua hospitali aliyolazwa, wanaweza kufanya juu chini wamfikie na kumdhuru kwa mara nyingine. Hilo jambo hatutaki kabisa litokee,” alisema ndugu huyo.

NDUGU, WATOTO WAKE WAZUIWA KWENDA UJERUMANI

Habari zaidi zinabainisha kuwa ndugu wa Said walipanga kwenda Ujerumani kumtembelea lakini walizuiwa kwa sababu awamu hii, viongozi wa familia yake wamezingatia usiri.

“Kuna watoto wake walikwenda Afrika Kusini na walikuwepo wakati anasafirishwa kwenda Ujerumani lakini waliambiwa warudi Tanzania kwa sababu kule Ujerumani utaratibu umebadilika.
 
Watu wachache wanaohusika na huduma pamoja na usalama wake ndiyo pekee wanaoruhusiwa,” alisema, akaongeza:

“Wapo ndugu wengine kutoka Saudi Arabia na Oman, vilevile nao wamezuiwa kwenda Ujerumani kumwona. Ni katika kuhakikisha mambo hayawi kama ilivyokuwa Afrika Kusini, maana kule ilishakuwa hatari, ndugu wengine wanaingia wodini, wanampiga picha na kusambaza mitandaoni. Safari hii mambo hayo hayatakiwi.”

APELEKWA UJERUMANI BAADA YA JK

Imeelezwa kwamba Said alipelekwa Ujerumani wiki moja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete kwenda kumtembelea alipokuwa amelazwa kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.

Dk. Kikwete, alikuwa kwenye ziara ya kikazi nchini Afrika Kusini alipokwenda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini ya Afrika (SADC), kuhusu pande tatu za umoja huo (Troika of SADC), hivyo kupata fursa ya kwenda kumjulia hali.

MUNGU AMPONYE SAID

Dawati la gazeti hili linamuombea Said apone kwani alionesha moyo wa ukarimu kwa familia 655 zilizokumbwa na mafuriko eneo la Jangwani, Desemba, 2011 kisha kuhamishiwa Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

MTUHUMIWA BADO KUKAMATWA

Kwa mujibu wa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Dar es Salaam, ACP Camillius Wambura alisema kwamba jeshi la polisi linaendelea kufanya kazi kwa nguvu na umakini mkubwa lakini mpaka sasa halijafanikiwa kumpata mtuhumiwa.

0 maoni:

Post a Comment

Labels