Jana majira ya saa mbili usiku, msanii na mchekeshaji maarufu nchini
Sharo Milionea amefariki dunia kwa ajali mbaya ya gari wakati akitoa Dar
es Salaam kueleka wilayani Muheza, Tanga.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Costantine Massawe
Hussein Ramadhani au Sharo Milionea alikuwa akiendesha gari namba T478
BVR Toyota Harrier.
Alipofika maeneo ya Segera gari lake liliacha njia
na kupinduka mara kadhaa, likagonga mti na kusababisha kifo chake na
yeye kutokea mbele ya kioo cha gari na kutupwa mbali.
Alisema Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali Teule ya
wilaya ya Muheza. Aliongeza kuwa hakuna kona kali wala ubovu wa
barabara kwenye sehemu aliyopata ajali.
Gari lake imehifadhiwa mahali
salama kwakuwa limeharibika vibaya na kwamba kwenye gari alikuwa
mwenyewe.
Habari kuhusu kifo chake zilianza kuenea jana usiku ambapo kwa upande
wa rafiki yake wa karibu Kitale amesema alikuwa akiipiga simu ya Sharo
Milionea iliyokuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa na kisha
kupigiwa simu na Tundaman, Mzee Majuto na Mjomba wake Sharo kumtaarifu
juu ya kifo hicho.
“Sisi binadamu tunaweza kuwaza hivi na Mungu naye akawaza lake
kwahiyo sisi tunaziombea familia hizi Mungu azipe faraja ya kweli na
faraja ya kweli nadhani inatoka kwa Mungu,”rais wa Shirikisho la Filamu
Tanzania , TAFF Simoni Mwakifwamba ameiambia TBC.
Kwa upande wake Steve Nyerere amesema kifo cha Sharo Milionea
kimetokea wakati ambao alikuwa ameanza kufanikiwa. “Sharo umri wake na
mambo aliyoanza kuyafanya ni makubwa.
“Sharo alishaanza kupata matumaini
yaani ni sawasawa unatupa mbegu halafu uitegemee inaanza kuchepua.
Sharo alishaanza kuchepua, anachepua ile mbegu yake, ameanza kujisaidia
yeye kama yeye sababu katika maisha lazima kwanza uanze kujisaidia wewe
kama wewe halafu pili uingalie jamii inahitaji nini kwako.
Amejipatia
usafiri maskini ya Mungu, pa kulala, na maisha yote ya kutoka Dar es
Salaam kwenda Tanga kuwaona wazazi kutumia gharama yake.”
Steve amesema jambo la msingi ni kumwachia Mungu na kuondoa mawazo mabaya kuhusiana na kifo chake.
Umoja wasanii wa filamu nchini umesema umepata pigo kubwa hasa
kwakuwa bado wana msiba wa msanii mwingine wa filamu, John Stephano
ambaye anatarajia kuzikwa leo.
Umesema baada ya mazishi hayo kesho
watasafiri kwa mabasi mawili kuelekea wilayani Muheza kwaajili ya
mazishi.
0 maoni:
Post a Comment